Page 37 - Kiswahili Grade 5 Yaliyomo ya kidijitali
P. 37
Miti husafisha hewa. Miti hutoa hewa ya oksijeni
ambayo viumbe huitumia. Jamani, kupuuza kuitunza miti
ni sawa na kujiangamiza!
Halikadhalika, miti hutupatia vyakula na matunda.
Vyakula na matunda hustawisha maisha. Chanzo kikubwa
cha vyakula vyetu ni miti.
Nani asiyejua kuwa baadhi ya miti hutupatia dawa?
Dawa nyingi za kutibia watu na mifugo hutokana na miti.
Mfano mzuri ni mti wa mwarobaini.
Miti hutupatia bidhaa nyingi tunazozitumia
katika maisha ya kila siku. Hata vitabu na madaftari
tunayoyatumia yametokana na miti. Je, samani
unazozitumia shuleni na nyumbani zimetokana na nini?
Vilevile, miti hutumika katika ujenzi.
Miti ina faida tele. Tunafaa kuipanda kwa wingi na
kuitunza. Hatuna budi kuepuka kukata miti kiholela.
Aidha, shughuli nyinginezo zinazochangia uharibifu wa
miti zinafaa kukomeshwa.
Sarufi
Umoja na wingi wa nomino za ngeli ya KU-KU
Sikiliza nomino za ngeli ya KU-KU zikisomwa.
Umoja Wingi
1. kusoma kusoma
2. kucheza kucheza
3. kulala kulala
4. kusimama kusimama
5. kulima kulima
6. kuandika kuandika