Page 20 - Kiswahili Grade 5 Yaliyomo ya kidijitali
P. 20
2. Juma alianza ufugaji kwa mbuzi mmoja. Alimnunua
mbuzi huyo kwa mkopo. Alifanya bidii kumlisha vizuri.
Wakati huo huo, alifanya vibarua mashambani mwa
wanakijiji. Alilipa mkopo na hata kujiwekea akiba.
Polepole, aliwanunua mbuzi wengine wawili. Mbuzi
wake walikomaa na kuanza kuzaana. Miaka michache
baadaye, Juma aliibukia kuwa mfugaji wa kutajika
ndani na nje ya kijiji chao. Watu walitoka mbali na
karibu kujifunza kutokana na ufugaji mbuzi wa Juma.
Ama kweli, anayejitahidi hufaidi.
3. Chuma hakufa moyo kupinga ukiukaji wa haki za
watoto kijijini. Aiwashauri wazazi kuwapeleka watoto
shuleni. Isitoshe, aliwahimiza waache tabia mbovu za
kuwaoza wasichana wao wachanga. Alizunguka kijijini
akiwashauri wazazi. Ilikuwa kazi ngumu na yenye
hatari lakini aliifanya. Wazazi wengi kijijini walianza
kuziheshimu na kuzitetea haki za watoto. Kweli, bidii
huleta ushindi.
4. Kijiji cha Kwea kilikuwa na shida chungu nzima
kutokana na uchafuzi wa mazingira. Chifu wa kata,
Bibi Tenda, aliwahamasisha wanakijiji kuyathamini
mazingira. Kila siku, alizunguka akiwaelimisha
wanakijiji. Alivuka milima na mabonde kuwafikia
wanakijiji wengi. Aliwasaidia kuzoa taka na kuzitupa
ifaavyo. Wakazi wengi walianza kumuunga mkono.
Nao walianza kuwaelimisha wenzao. Polepole,
uchafuzi wa mazingira ulitokomea kijijini. Kijiji cha
Kwea kikawa safi na mfano wa kuigwa. Kweli, mtaka
cha mvunguni sharti ainame.
5. Madaktari na wataalamu wa afya hawakufa moyo.
Waliongeza bidii katika utafiti wao. Walitumia wakati
mrefu na nguvu nyingi kugundua dawa ya ugonjwa
huo wa kutisha. Baadaye, walifanikiwa kupata dawa
ya kutibu ugonjwa huo. Ama kweli, ukiona vyaelea
vimeundwa.