Page 14 - Kiswahili Grade 5 Yaliyomo ya kidijitali
P. 14
“Garimoshi lilikuwa na mamia ya abiria. Je, nao
wangetungoja?” Babu Leposo alimwuliza Fuai.
Fuai alipata funzo muhimu tangu siku hiyo. Yeye
hujitahidi kufanya mambo wakati ufaao.
Kifungu 3
Soma kifungu kifuatacho.
Wakati upepo
Wanyama wote wa msituni walikuwa wameandaa
hafla ya kumtuza Mbweha. Mbweha angepewa taji la
kuwa mnyama aliyeonyesha huruma baada ya kumwokoa
mtoto wa Sungura alipozama mtoni.
Hafla yenyewe ilipangwa kufanyika siku ya Alhamisi.
Kila mnyama alifaa awe amefika uwanjani saa mbili
kamili asubuhi. Sherehe zilipangiwa kuendelea hadi saa
sita adhuhuri.
Siku ya hafla, Mbweha alikuwa amepanga kuamka
alfajiri. Aliamka saa moja na robo asubuhi. Alijitayarisha
haraka na kuondoka mwendo wa saa moja na nusu.
Alitimua mbio kuelekea shereheni. Ghafla, aligundua
hakuwa amebeba kadi ya mwaliko. Lazima angerudi
kuichukua.
Alirudi mbio hadi kwake. Alianza kuitafuta kadi ya
mwaliko. Hakukumbuka mahali aliiweka. Baadaye,
aliipata. Alipoangalia saa, ilikuwa ni saa mbili na dakika
tano asubuhi.
Mbweha aliamua kupitia njia ya mkato kwenye
shamba la Mzee Kiomo. Njia hiyo ilikuwa hatari. Mbweha
hakujali. Alishika njia ya mkato.