Page 46 - Kiswahili Grade 5 Yaliyomo ya kidijitali
P. 46
Miezi michache baadaye, mambo yalianza kubadilika.
Watoto wa Mzee Kosi walianza kukosa kuhudhuria
masomo siku za Jumatatu na Jumanne. Aliwatetea kwa
kusema kuwa walihitaji kupumzika baada ya maombi na
shughuli nyingi za Jumapili. Mwalimu mkuu aliwaita Mzee
Kosi na mkewe shuleni na kuwashauri kutotatiza masomo
ya wana wao.
Baada ya miezi kadhaa, watoto wa Mzee Kosi walikosa
kufika shuleni kabisa. Mwalimu mkuu na walimu wa
madarasa ya watoto wale walienda nyumbani kwa Mzee
Kosi kuchunguza kiini. Waliwashawishi na kuwashauri
wazazi wale kuwaruhusu watoto wasome. Mambo
yalipogonga mwamba, walipiga ripoti kwa chifu wa eneo
lao.
Chifu alifika nyumbani kwa Mzee Kosi. Alipigwa
na butwaa. Maskini watoto wa Mzee Kosi walikuwa
wamefungiwa chumbani! Walikuwa wakikariri vifungu
vya maneno kutoka kitabu fulani cha kidini. Chifu alitaka
kujua ni kwa nini watoto wale hawakwenda shuleni.
“Imani yetu haituruhusu kufanya hivyo,” Mzee Kosi
alimwambia chifu.
“Hamuoni mnawanyima haki ya elimu watoto hawa
kwa kisingizio cha imani?” Chifu alichemka.
Mzee Kosi na mkewe hawakuwa na maneno ya
kujitetea.
Chifu alihakikisha watoto wa Mzee Kosi wamerudishwa
shuleni. Mzee Kosi na mkewe walipewa ushauri nasaha.
Mwishowe, walitoka gizani na kutupilia mbali mafunzo ya
dhehebu hilo la ajabu.